Thursday, 20 November 2014

shy-rose bhanji adaiwa kumpiga mbunge mwenzake

Dar es Salaam. Mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji
ameingia katika mgogoro mpya baada ya
kutuhumiwa kumpiga mbunge mwenzake
kutoka Tanzania
, Dk Nderakindo Kessy
jijini Nairobi, Kenya.
Bhanji, ambaye amekuwa katika mgogoro
na wabunge wenzake kwa kipindi cha
miezi miwili sasa, anadaiwa kumvamia
Dk Kessy na kumpiga mgongoni.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi,
Dk Kessy alisema tukio hilo lilitokea
bungeni juzi jioni baada ya kikao
kuahirishawa.
“Kwa kuwa muda wa Bunge ulikuwa
umeisha nisingeweza kuipeleka kesi hiyo
bungeni badala yake ikawa shambulizi na
niliambiwa kiutaratibu nikaripoti Kituo
cha Polisi cha Bunge ambako baadaye
nilikwenda na kupatiwa cheti cha
matibabu,” alisema Dk Kessy.
Alisema baada ya kupatiwa cheti cha
matibabu na polisi alikwenda katika
Hospitali ya AAR jijini humo ambako
alipimwa na kupewa majibu
aliyoyapeleka polisi kwa uchunguzi.
Hadi tukio hilo linatokea, alisema hakuwa
amekwaruzana na Bhanji zaidi ya
kushangaa akimvamiwa.
Baada ya kunipiga hakukuwa na
madhara ya papo kwa papo kama alama
yoyote mwilini au damu ila nayasikia
maumivu, sijui hapo baadaye,” alisema
Mbunge huyo ambaye ni kada wa NCCR-
Mageuzi.
Bhanji hakupatikana jana kuzungumzia
tuhuma hizo, kwani simu yake ilikuwa
imezimwa na hata ujumbe wa barua pepe
alioandikiwa hakurudisha majibu. Ofisa
Uhusiano Mwandamizi wa Eala, Bobi
Odiko alisema: “Nimesikia kwamba
mmoja ya wabunge alimpiga mwenzake
kipepsilakini ilikuwa nje ya Bunge,
bado ninaendelea kutafuta ukweli wa
kina juu ya tukio hilo.”
Bunge la Eala, tangu mwanzoni mwa
mwaka huu, limekuwa likitawaliwa na
vioja na mivutano ya hapa na pale na
mikakati ya kumng’oa Spika Magreth
Zziwa kwa madai ya kutofanya kazi kwa
weledi.
Hivi karibuni, Bhanji aliliingiza Bunge
hilo katika mvutano baada ya kudaiwa
kuliaibisha wakati wa ziara ya Ubelgiji
iliyowashirikisha wajumbe wa tume na
wenyeviti wa kamati za Bunge hilo.
Alituhumiwa kufanya fujo ndani ya ndege
kwa kutoa lugha chafu kwa wabunge
wenzake na matamshi yasiyo ya staha
katika hafla iliyoandaliwa na Balozi wa
Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus
Kamala.
Baada ya tukio hilo, baadhi ya wabunge
walitaka Bhanji achukuliwe hatua za
kinidhamu.
Hali hiyo ilifanya vikao vilivyokuwa
vikifanyika jijini Kigali, Rwanda mwezi
uliopita kuahirishwa kila baada ya dakika
20 au 30 kutokana na wabunge kutumia
kanuni ya 31 kutoa hoja zao kutaka
mjadala kuhusu Bhanji ufanyike kwanza
kabla ya kuendelea na kazi nyingine.
Bhanji alikanusha tuhuma zote na kuziita
uzushi na zenye nia ya kuzimisha juhudi
zake za kupinga njama ovu za kumng’oa
Spika Zziwa.
Kabla ya Bunge hilo kuanza Nairobi
Novemba 14, Bhanji aliandika kwenye
ukurasa wake wa Facebook: “Kwa
Tanzania kuna sahihi mbili tu… lengo
kubwa la kumwondoa Spika ni sehemu ya
‘mchezo mchafu ili kikundi fulani’
wamuweke Spika mwingine kwa masilahi
ya wachache.”
Hata hivyo, bado haijabainika wazi iwapo
hatua ya kumvaa Dk Kessy ilikuwa ni
sehemu ya mvutano huo kwani Dk Kessy
alisema hajui chanzo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia alisema wamepata taarifa za tukio
hilo na wamezipa umuhimu mkubwa na
kimeshafikisha malalamiko rasmi kwa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta.
Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania
ndani ya Eala, Adam Kimbisa alisema
hakuwa ameambiwa chochote juu ya
tukio hilo... “Nipo kwenye kikao.
Sijaambiwa chochote.” Alipoulizwa iwapo
alikuwa na taarifa za awali juu ya tukio
hilo alisema: “Sina uhakika na habari
hizo.”
Waziri Sitta alikiri kusikia tukio hilo na
kubainisha kuwa lilitokea kwa bahati
mbaya wakati Bhanji anapita katika kundi
la wabunge na kumgonga Dk Kessy na
kwa kuwa alikuwa na haraka hakuweza
kusimama.
Alisema Kwa kuwa Dk Kessy hakupata
maumivu makali wabunge hao jana
asubuhi walikaa pamoja na kuelewana.
Aliongeza kuwa taarifa rasmi kutoka kwa
naibu wake, Dk Abdallah Sadala aliyepo
Nairobi, ni kwamba baada ya maelewano
hayo Sajenti wa Bunge alikwenda kituoni
hapo kueleza kwamba Bhanji hakufanya
kitendo hicho kwa makusudi na walikuwa
wamemalizana.

No comments:

Post a Comment